Mike Tyson amepona sasa

MIKE TYSON AMEPONA SASA!
MEI 23, 2017, Mike Tyson, kupitia jukwaa la Salt Conference, CNN, alisema: "Sikudhani kama ningeuvuka umri wa miaka ya 30." Tyson alidhani angekufa kwa sababu alikata tamaa, kila kitu kilegeuka juu chini, akawa chapombe, mvuta bangi na mbwia unga.
Ajabu eeh! Tyson aliyashinda maisha akiwa na umri wa miaka 15. Akatwaa medali ya Olympic. Akatwaa nyingine akiwa na miaka 16. Akawatwanga "baba zake" ulingoni akiwa na umri wa miaka 18. Tyson mwenye miaka 20, alitwaa ubingwa wa dunia wa boxing. Umri mdogo zaidi kupata kutokea.
Mwenye ngumi katili. Aliyepanda ulingoni kuua, sio kuburudisha. Alikuwa na afya imara kweli. Mwaka 1985 alipigana mapambano 15 ndani ya miezi 9. Wastani wa pambano moja kila wiki mbili na alishinda yote. Ngumi zilimpenda, mashabiki walimpenda, fedha zilimkimbilia kwa fujo.
Maisha ya starehe na fujo za ujana, vilipunguza umwamba wake. Katika documentary inayoitwa "Tyson" ya mwaka 2008, Tyson alisema, mapambano ya mwishoni kabla ya kustaafu, alijilazimisha sababu ya ukata, lakini hakuwa na uwezo! Na alipigika kweli, pambano na McBride mwaka 2005, aliomba poo raundi ya sita!
Tyson alikuwa na madeni kibao na aliuza kila kitu chake cha thamani kubwa. Mijengo ya kifahari, magari, mikanda ya boxing mpaka medali zake za dhahabu.
Tyson wa kuishiwa? Mwaka 2000 pekee aliingiza dola 65.7 milioni (Sh153.7 bilioni). Hiyo ni sawa na Sh12 bilioni kila mwezi. Sh429 milioni kwa siku. Sh18 milioni kwa saa. Hiyo ni mwaka mmoja, tena wakati huo hakuwa Tyson wa kutisha.
Maisha ya kifahari huunguza pesa mithili ya petroli kwenye V8. Kuanzia mwaka 2003 Tyson alianza kuishi kwa tabu. Alipoacha kupigana ndio ikawa balaa, akawa teja.
Sikia, nyakati za maumivu na kukata tamaa, unahitaji mtu wa kukushika mkono na kukupa moyo. Angalau akwambie kwa kukunong'oneza kuwa maisha hayajafika mwisho.
Mrembo Lakiha Spicer 'Kiki' alikuwa rafiki wa muda mrefu wa Tyson. Kipindi Tyson akioneka amefulia, Kiki alimuona ni mwanaume mzuri. Aliamini anajitaji kutulizwa na kila kitu kingekuwa sawa.
Tyson alifunga ndoa na Kiki Juni 2009. Kuanzia hapo, kazi ya Kiki ikawa kumfumbua macho Tyson ili aache kulalamika giza, aone mwanga. Tyson akaanza kuyaona maisha upya.
Tangu wakati huo, Tyson ameandika vitabu na kuingiza mamilioni ya dola, ametengeneza documentaries, amecheza movie, amesaini mikataba na kuingia hisa na makampuni ya matangazo pamoja na promosheni za boxing. Kwa sasa Tyson yupo vizuri, kipesa na kiakili. Ni mtu mzima sasa. Miaka 52 kwenye akaunti ya umri. Analea vizuri watoto wake saba!
Juzijuzi alikuja na mradi wa ranchi ya bangi. Eka zaidi ya 400. Kutakuwa na hoteli. Vilevile bangi itavutwa ki-VIP na kuuzwa ki-7Star.
Anyways, mambo ya bangi achana nayo, japo ni mradi wa pesa nyingi. La kuchukua ni hili, nyakati za kujiona umefeli, unahitaji mtu akupe moyo, akwambie "maisha hayafika mwisho". Hata ukiwa vizuri sana, tambua pia maisha hayajafika mwisho. Huna wa kukwambia? Jiambie mwenyewe!
Ndimi Luqman MALOTO

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZA KUOA MKE ALIEKUZIDI UMRI

HISTORIA YA KHALIFA WA PILI SAYYIDNA OMAR (R.A)

Elimu kwa wanawake