Namna ya Kuandaa Mchanganuo wa biashara



Maana ya na umuhimu wa mchanganuo
Mchanganuo wa biashara ni andiko ambalo linaweka bayana malengo na madhumuni ya biashara na namna yatakavyofikiwa. Ni mpangilio maalum wa kuongoza utekelezaji wa kufanikisha lengo la biashara.
Kuandaa mpango wa biashara ni muhimu kwa mafanikio ya biashara yoyote. Mchanganuo wa biashara hutoa dira na kusaidia kuongoza uendeshaji wa biashara. Mara nyingi ni sharti mojawapo katika kuomba mkopo.
Mpango wa biashara ulioandaliwa vizuri utatoa majibu ya maswali mbali mbali kama vile nini madhumuni ya biashara yako, Utamwuzia nani/akina nani? Ni yapi malengo yako ya mwisho? Utagharimia vipi biashara yako? na mengine mengi
Mpango wako wa biashara utakusaidia kutafakari mwelekeo wa kampuni yako na namna ambavyo itakabiliana na changamoto mbalimbali ili iwe endelevu.
Vipengele muhimu vya Mchanganuo wa Biashara
Vipengele muhimu vya Mchanganuo wa Biashara ni kama vifuatavyo:-
1. Ufupisho
Kipengele hiki huandikwa mwishoni. Andika katika kipengele hiki mambo ambayo ungeandika kama ungeambiwa uelezee biashara yako kwa dakika tano katika usaili. Iandike kitaalamu, kiukamilifu, kwa usahihi, na kuonesha hali ya juu ya kujiamini.
Elezea mambo ya msingi kuhusu biashara: Bidhaa yako ni nini? Wateja wako ni kina nani? Wamiliki ni kina nani? Unafikiri nini kuhusu mustakabali wa biashara yako na tasnia yake kwa ujumla?
Ikiwa unaomba mkopo, eleza ni kiasi gani unahitaji, fafanua kiasi hicho kitatumikaje, na namna kitakavyosaidia katika kuboresha biashara yako.
Muhtasari ni lazima uwe ni jumuisho la vitu vifwatavyo:
• Mpango wa biashara unahusu nini
• Bidhaa au huduma inayoletwa na umuhimu wake
• Upatikanaji wa masoko
• Mpangilio wa uongozi
• Matarajio ya kifedha
• Fedha zina hozohitajika na mapato yake
2. Maelezo ya Biashara
Unaingia kwenye biashara gani? Utafanya nini? Kwa kifupi, wateja wako ni akina nani? Taja ni wapi eneo lako la biashara na saa za kazi ni zipi.
Biashara itakuwa katika muundo upi wa umiliki kisheria: Mfanyabiashara pekee, ubia, shirika, kampuni yenye ukomo wa madeni? Kwa nini umechagua muundo huo?
Wamiliki wakubwa wa biashara ni kina nani? Elezea sifa zao kwa kifupi.
Malengo ya kampuni: Unatarajia kampuni yako iwe katika hatua gani ndani ya mwaka wa kwanza? Na baada ya miaka 3-5.
Falsafa ya Biashara: Ni jambo gani muhimu kwako katika biashara? Mambo gani yatasaidia kampuni kufanikiwa?
Una uwezo mzuri katika Nyanja zipi za kiushindani? Kundi gani katika soko unalenga kulitumia kufanikisha kuingia sokoni.
Maelezo juu ya uzalishaji (kama upo) na mahitaji
3. Utawala na uendeshaji (kurasa 1-2)
Taja jina la biashara, muundo wa kisheria na umiliki: Mfano “ ABC ni ni biashara inayoendeshwa na mmiliki mmoja pekee na inamilikiwa na Jane Success.”
Elezea kwa kifupi kuhusu mmiliki na sifa zinazomuwezesha kuendesha biashara hiyo. Ambatanisha wasifu wa kila mmiliki.
Nani atafanya kazi ipi? Kama utafanya mwenyewe kila kitu, elezea namna utakavyofanya shughuli za ununuzi, masoko, utunzaji wa mahesabu, wateja, mali, ukarabati, n.k.
Utakuwa na waajiriwa? Watafanya kazi gani? Watahitaji kuwa na sifa gani? Utawalipa kiasi gani? Kuna mpango wowote wa mafunzo?
Utatumia wataalamu kutoka nje au wanafamilia kusaidia uendeshaji? Onesha iwapo watakuwepo wahasibu, watunza kumbukumbu za fedha, wanasheria, n.k. Elezea wanafamilia watachukua majukumu gani katika biashara.
Biashara yako inahitaji leseni maalum, au inabanwa na sheria/ kanuni/ makubaliano maalum? Eneo ilipo biashara ni sahihi kisheria kwa ajili ya uuzaji au uzalishaji unaofanyika? Una bima ipi katika biashara yako?
Bainisha wauzaji wako wakuu. Una wauzaji wengine wa kutegemea ikiwa ulionao watashindwa kukuuzia?
Utauza kwa mkopo? Utaweka vigezo na masharti gani kwa wateja wanaokopa bidhaa/ huduma? Utapimaje uaminifu wa mteja mpya?
4. Masoko
Katika kipengele cha masoko unatakiwa uelezee mambo kadha wa kadha kama ilivyobainishwa hapa chini.
a. Picha ya jumla ya sekta
Unafahamu kiasi gani kuhusu sekta ya biashara yako? Biashara inakua kwenye hiyo sekta? Kuna mabadiliko gani yanayoendelea? Soko likoje katika eneo unapopanga kuendesha biashara yako?
b. Soko unalolenga
Elezea soko la msingi unalolenga katika biashara yako. Hawa ndio wateja wako muhimu kuliko wote. Chambua wateja wako kwa vigezo kama umri, jinsia, kipato. Wateja wako wako maeneo gani? Wateja wengine unaowalenga ni wapi?
c. Ushindani
Orodhesha washindani watatu wakubwa ambao unashindana nao moja kwa moja (wanaofanya biashara inayofanana na ya kwako).
Watashindana nawe katika kila kitu au katika baadhi tu ya bidhaa, wateja au maeneo?
Wana nguvu gani ya ziada kukuzidi? Na utakabiliana vipi na hali hizo?
Wana madhaifu gani? Na utatumiaje madhaifu yao kwa faida yako?
Unalenga kundi gani katika soko? (Usijaribu kutaka kufanya kila kitu kwa kila mteja)
d. Bidhaa/Huduma
Elezea kwa kirefu huduma unayotoa au bidhaa unazouza.
e. Kuvutia wateja/Kutangaza biashara
Utawafikishia vipi wateja ujumbe? (elezea iwapo utatumia matangazo ya maandishi/ picha, maonesho ya biashara, wavuti, vipeperushi, kadikazi, mawasiliano ya barua, mitandao mbalimbali, ya kijamii, n.k). Kadiria gharama na tarehe, idadi ya matangazo, n.k.
f. Kupanga bei
Umefanyaje maamuzi kuhusu bei? Bei zako zinaendana na soko? Bei zako zikoje ukilinganisha na za washindani wako?
g. Eneo la biashara
Unafanyia wapi biashara yako? Nyumbani? Ofisini, au dukani? Eleze sababu za uchaguzi wake. Ikiwa bado hujafikiria au hujafanya maamuzi, elezea unatafuta eneo la namna gani.
5. Mipango ya kifedha
Katika kipengele hiki, elezea masuala mbali mbali ya kifendha ikijumuisha
a. Taswira yako binafsi ya kifedha, Makadirio/ matarajio ya kifedha , kwa ajili ya mashine, vifaa, ofisi, n.k.
c. Gharama za kuanzia na vyanzo vya fedha: mfano wa vyanzo vya fedha ni akiba yako mwenyewe, marafiki, wawekezaji, mikopo, n.k.
d. Matumizi ya fedha na dhamana
e. Taarifa ya mapato, na taarifa ya hali ya kifedha (faida na hasara).
f. Mtiririko wa fedha taslimu (kiasi kinachoingia na kutoka katika biashara kwa kipindi fulani – mwezi)),
Viambatanisho:
• Matarajio ya kifedha ya kina kwa mwezi
• Wasifu wa wafanyakazi wa muhimu
• Taarifa za utafiti wa masoko
• Mpangilio wa uongozi
Kwa maelezo zaidi:
• Toviti: www.wajasiriamalitz.or.tz
• USSD code *148*99*06#
Imeandaliwa na Veneranda Sumila
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZA KUOA MKE ALIEKUZIDI UMRI

HISTORIA YA KHALIFA WA PILI SAYYIDNA OMAR (R.A)

Elimu kwa wanawake