Mjue Bi Khadija binti Khuwailidi mke wa kwanza wa Mtume

MFAHAMU:

                                       
 KHADIJA BINT KHUWAILYD
                             MKE WA KWANZA WA MTUME MUHAMMAD:

Bibi Khadijah Bint Khuwaylid (R.A) alikuwa ni mwanamke bora kuliko wanawake wote wa wakati wake. Alikuwa ni binti ya Khuwaylid Bin Asad Bin Abd il-'Uzza Bin Qusayy Bin Kilab kutokamana na Quraysh. Kabla ya Uislamu, alikuwa akiitwa atTwaahira (msafi). Khadijah alikuwa ni mwanamke tajiri, hivyo basi, akamuajiri Mtume (S.A.W) kuisimamia biashara yake ya msafara kuelekea Sham. Baada ya kushuhudia uaminifu wake na usimamizi mzuri, Bibi Khadijah alijitolea nafsi yake ili aolewe na Mtume (S.A.W), Mtume akakubali kumuoa.

Kabla ya kuolewa na Mtume (S.A.W), aliolewa na Abu Halah Bin Zurarah at-Tamimi, kisha akaolewa na 'Atiq Bin 'Abid Bin 'Abdillah Bin 'Umar Bin Makhzum. Mtume (S.A.W) alipomuowa Bibi Khadijah,Mtume alikuwa na umri wa miaka ishirini na tano nae Bibi Khadijah alikuwa na miaka arubaini.
Alimzalia Mtume (S.A.W) watoto sita; waume wawili(Al-Qasim,na abdillah) na wanawake wanne (Ruqayyah,Zaynab,Umm Kulthum na Faatimah). Watoto wa kiume walifariki mapema katika hali ya utoto na watoto watatu wakwanza wa kike walifariki wakiwa al-Madina wakati wa uhai wa Mtume (S.A.W). Faatimah (R.A.) alifariki miezi sita baada ya Mtume kufariki.

Bibi Khadijah ndie mtu wa kwanza kabisa kumuamini Mtume (S.A.W) na kumsaidia. Mara kwa mara Jibril (A.S.) alikuwa akimuuliza Mtume (S.A.W) amsalimie Bibi Khadijah: "Ewe Khadijah, Jibril akusalimu." "Ewe Muhammad, mwambie Khadijah asalimiwa na Mwenyezi Mungu." Khadijah ni mmoja kati ya wanawake wanne walotajwa na Mtume (S.A.W) kuwa wamekamilika: "Walokamilika miongoni mwa wanaume ni wengi (kwa Imani, Tabia na Taqwa), lakini wanawake (wanne tu) ndio walokamilika: Asiyah mkewe Fir'auni, Maryam Bint 'Imran,Khadijah Bint Khuwaylid na faatwima na ubora wa ''Aaisha juu ya wanawake wengine ni kama ubora wa tharid juu ya aina nyengine ya chakula."

Mtume (S.A.W) hakuwahi kuowa mwanamke mwengine kabla ya Khadijah na wala hakuongeza mke mwengine wakati alipokuwa nae. Alipokufa alikuwa na majonzi makubwa sana na mwaka alokufa uliitwa 'MWAKA WA MAJONZI'

Aaisha (R.A.) akasema yakwamba alipokuwa Mtume (S.A.W) akimtaja Khadijah, jambo hilo lilikuwa halimchoshi na akimsifu na kumuombea msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu . Siku moja wivu wake ulimzidi akasema, "Mwenyezi Mungu amekupa alie bora kuliko huyo mwanamke mzee." Aaisha aliziona alama za kughadhibika juu ya uso wa Mtume (S.A.W). Akahisi kuwa amekosea kutamka hivyo..... Mtume akamwambia "Aaisha vipi utasema hivyo! Wallahi, yeye ameniamini mimi wakati watu waliponikataa, na akanihifadhi mimi wakati watu waliponifukuza. Na nimebarikiwa na watoto kutokamana na yeye, ambapo nyinyi (wake wengineo) mumenyimwa kupata watoto kutokamana na mimi."
Akasema Aisha, "Aliendelea kuyakariri maneno hayo, usiku na mchana, kiasi cha mwezi mzima.
Bibi Khadijah ana daraja bora miongoni mwa wanawake waislamu wa nyakati zote. Hiyo ni kwa sababu hakuwa na msimamo wa kusitasita alipokuwa akimsaidia mbora wa waume alowahi kuwa nao. Alimuamini , akajitolea kwa hali na mali juu yake; na akampa moyo kwenye wakati wa mashaka. Mwenyezi Mungu alimjaaliya pepo kwa msimamo alokuwa nao kwenye maisha ya Mtume (S.A.W), na kwa sababu hiyo katika maisha ya kila muislamu. Mtume (S.A.W) alikuwa akiuenzi ukumbusho wake na kuudumisha uhusiano na marafiki zake baada ya kufa kwake. Mwenyezi Mungu akamjaalia kupata nafasi yakuwa mama wa watoto wote wa Mtume (S.A.W). Wanawake wote waislamu wanatakiwa wafaidike kutokamana na mfano wa Bibi Khadija.
Bibi Khadijah (R.A.) alikufa miaka mitatu
 kabla ya kuhama mtume kwenda madina, na akazikwa mahala paitwapo Al-Hajun (mlima juu ya Makkah). Nae akifa alikuwa na umri wa miaka sitini na tano.
💓💓💓
RAMADHAN KAREEM.

Comments

Popular posts from this blog

FAIDA ZA KUOA MKE ALIEKUZIDI UMRI

HISTORIA YA KHALIFA WA PILI SAYYIDNA OMAR (R.A)

Elimu kwa wanawake